Mto

mkondo mkubwa wa maji wa asili
Pitio kulingana na tarehe 08:38, 28 Machi 2012 na Idioma-bot (majadiliano | michango) (r2.7.2) (Roboti: Imeongeza lez:ВацІ)

Mto ni mwendo asilia wa maji yanayofuata njia yake kwenye mtelemko hadi mdomoni wake.

Mto wa Nile nchini Misri

Chanzo

Chanzo cha mto mara nyingi ni chemchemi au ziwa au maungano ya vijito vidogo. Mto hufuata mwendo wake kwa mtelemko hadi mwisho wake baharini au ziwani au kwa mto mwingine. Kama mto ni mdogo huitwa kijito. Mto mkubwa sana kama Kongo au Nile unaweza kuitwa mto mkubwa au jito.

Lalio chini ya mto

Njiani yake mto huwa umechimba lalio linalofanana na mfereji kati ya udongo au mawe ya kingo zake. Nguvu ya kusogeza maji mtoni ni uvutano wa dunia.

Mdomo na delta

Mwisho wa mto huitwa mdomo. Mdomoni kwa kawaida mto huishia katika gimba kubwa zaidi ya maji, ama mto mkubwa au ziwa au bahari. Mdomo huu unaweza kuwa pana kama kijazio hasa baharini ambako bahari inapanuka wakati wa maji kujaa.

Mito mingine inaonyesha mdomo wa delta kama imegawanyika mdomoni kuwa na mikono mingi inayoelekea bahari kwa umbo la pembetatu.

Tawimito na jina

Njiani mito mingi inaunganika kuwa mito mikubwa zaidi. Ni desturi kutumia jina la mto ulio mkubwa zaidi mahali pa kuungana kwa ajili ya sehemu inayofuata ya mto uliopanuka.

Kwa mfano mito ya Ubangi na Kongo zinakutana kwa mji wa Mbandaka. Hapa Kongo ni mto mkubwa kushinda Ubangi; pia baada ya Mbandaka kuelekea bahari mto unaendelea kuitwa "Kongo".

Wakati mwingine ni swali la uzoefu tu jinsi ya kutaja mto; Kongo inaitwa Lualaba hadi mji wa Kisangani. Wataalamu wengine wanasema ya kwamba mto Kagera ingestahili kuitwa "Nile" kwa sababu ni mto uleule unapita tu kwenye ziwa Viktoria Nyanza.

Kuna pia uzoefu ambako jina la mto mdogo linaendelea kutumikwa. Mto Ruvuma unatoka Songea na kufuata mpaka wa Tanzania na Msumbiji. Inakutana na mto Lujenda ambayo ni mto mkubwa zaidi; inawezekana kusema ya kwamba Ruvuma inaingia Lujenda lakini jina la Ruvuma linatumika hadi mdomoni.

Mito midogo zaidi inayojiunga na mto fulani huitwa tawimito.

Beseni

Jumla ya eneo ambako tawimito yote hata vijito asilia kabisa zinaanza na kupokea maji yao huitwa beseni ya mto. Sehemu kubwa ya Tanzania ya kaskazini-magharibi ni sehemu ya beseni ya Nile kwa sababu matone ya mvua kama yanafika mtoni yote huelekea ziwa Viktoria Nyanza na kuingia mto Nile kwenda bahari ya Mediteranea.


Mito katika dura ya maji duniani

Mito inabeba kiasi kikubwa cha maji ya mvua ikirudi baharini katika dura ya maji duniani.

Maji ya mtoni ni maji matamu tofauti na maji ya chimvi baharini. Hii ni sababu ya kwamba mimea, wanyama na watu hupenda kukaa karibu na mito.

Watu huona faida zaidi kwa sababu mito mikubwa na majito inafaa pia usafiri. Kihistoria mito ilikuwa kati ya njia za kwanza kabisa za mawasiliano kati ya maeneo ya mbali.

Mito kumi mirefu duniani

Kadirio ya urefu wa mto hutegemea jinsi ya kuhesabu tawimito yake. Orodha inayofuata ina tofauti na orodha inayokadiria kwa namna nyingine.

  1. 6.671 km - Nile: Luvironza-Ruvuvu-Ruvusu-Kagera-Nile Nyeupe-Nile - (Afrika)
  2. 6.387 km - Amazonas: Apurimac-Ene-Tambo-Ucayali-Amazonas - (Amerika ya Kusini)
  3. 6.380 km - Yangtse (Cháng Jiāng) - (Asia)
  4. 6.051 km - Mississippi-Missouri - (Amerika ya Kaskazini)
  5. 5.940 km - Yenisei-Angara - (Asia)
  6. 5.410 km - Ob-Irtysch - (Asia)
  7. 5.052 km - Amur-Argun-Kerulen - (Asia) - (pekee wakati wa mvua nyingi)
  8. 4.845 km - Huang He - (Asia)
  9. 4.500 km - Mekong - (Asia)
  10. 4.374 km - Kongo - (Afrika)


Viungo

Mito mirefu ya Afrika


  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mto kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.

Kigezo:Link FA