Mtaguso wa nne wa Konstantinopoli
Sehemu ya mfululizo kuhusu |
Mitaguso mikuu ya Kanisa Katoliki |
---|
Mtangulizi (50 hivi) |
Roma ya Kale (325–451) |
Mwanzoni mwa Karne za Kati (553–870) |
Mwishoni mwa Karne za Kati (1122–1517) |
Nyakati za uvumbuzi mwingi (1545–) |
Mtaguso wa nne wa Konstantinopoli ni jina linalotumiwa na Wakristo kwa namna tofauti, kadiri wanavyokubali au kukataa uhalali na uekumeni wa mitaguso fulanifulani.
Kanisa Katoliki linahesabu kuwa Mtaguso mkuu wa nne ule uliofanyika tangu tarehe 5 Oktoba 869 hadi 28 Februari 870.
Uliitishwa na Kaisari Basili I wa Bisanti na Papa Adrian II (867-872) kwa sababu mwisho wa ikonoklastia katika sinodi ya mwaka 843 ulikuwa umeacha athari kubwa katika Kanisa la Mashariki.
Mazingira ya kihistoria
[hariri | hariri chanzo]Patriarki Metodi wa Konstantinopoli (843-847) alijitahidi kutuliza pande zote, lakini hakufaulu.
Alipofariki, malkia Teodora, akitawala kwa niaba ya mtoto Mikaeli III wa Bisanti alilazimisha nafasi yake ishikwe na Ignas I (847-858), mmonaki mwenye msimamo mkali, ambaye hatimaye aliondoshwa.
Badala yake alichaguliwa mlei msomi Fosyo ambaye kwa siku chache alipewa daraja na kutawazwa, lakini kufikia Februari 859 lililotea farakano kati ya waliomkubali yeye na waliomkubali Ignas I.
Ndipo Fosyo alipojitahidi kuungwa mkono na Papa Nikolaus I (858-867), ambaye kwanza alimkubali pamoja na pendekezo la Kaisari Mikaeli III la kuitisha mtaguso uliofanyika Konstantinopoli kati ya Aprili na Agosti 861 wakihudhuria maaskofu zaidi ya 300.
Papa hakupendezwa na maamuzi ya mtaguso huo, akashindana na Kaisari kimaandishi kwa sababu za kiutamaduni na za kisiasa pia.
Hapo Fosyo alipata nguvu dhidi ya Papa akaitisha mtaguso uliovunja umoja kati ya Makanisa ya Mashariki na yale ya Magharibi mwaka 867, akithubutu kwa mara ya kwanza kumhukumu Papa kama mzushi na kutaka kumuondoa madarakani.
Kumbe Kaisari mpya alimrudisha Ignas I kuwa Patriarki na pamoja naye akamuomba Papa atume mabalozi kwa mtaguso mwingine wa kufanyika Konstantinopoli.
Mtaguso ulipoanza tarehe 5 Oktoba 869 walikuwepo tu maaskofu wakuu 5 na maaskofu wengine 7, lakini walikuwepo mabalozi wa Mapatriarki wa Antiokia na Yerusalemu (wale wa Aleksandria walifika baadaye).
Waliokuwa upande wa Fosyo walikubaliwa kuhudhuria kuanzia tarehe 7 Oktoba wakamtetea sana dhidi ya msimamo wa Papa, lakini wakashindwa na kutengwa (29 Oktoba).
Baada ya miezi mitatu mtaguso uliendelea tarehe 12 Februari 870, wakiwepo maaskofu 67 walioongezeka tena hadi kufikia 103 siku ya mwisho (28 Februari), lilipotolewa tamko la imani pamoja na kanuni 26 kuhusu teolojia na sheria, bila ya kutoa mafundisho mapya. Pamoja na idadi yenyewe kutokuwa kubwa sana, ni muhimu kwamba walikuwepo maaskofu wakuu 37 kati ya 40.
Kwa kuwa mtaguso huu haukukubaliwa sana huko Konstantinopoli (hasa baada ya Fosyo kurudia Upatriarki mwaka 877), na pande mbili zilishindwa zaidi na zaidi kuelewana, uliitishwa mtaguso mwingine, ambapo wafuasi wa Fosyo walikuwa ndio wengi.
Baadhi ya Waorthodoksi wanahesabu mtaguso huo mpya (879-880), uliofuta maamuzi dhidi ya Fosyo, kuwa wa kiekumeni na kuukataa ule wa miaka 10 ya nyuma. Lakini wengine hawaukubali kuwa wa kiekumeni kwa sababu haukutoa mafundisho ya imani.
Ingawa wajumbe wa Papa Yohane VIII (872-882) walikubali kwanza maamuzi wa mtaguso huo ili kudumisha amani, na labda hata yeye mwenyewe, waandamizi wake waliukataa, na Fosyo mwenyewe aliondoshwa tena mwaka 886.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mtaguso wa nne wa Konstantinopoli kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |