Nenda kwa yaliyomo

Rasi ya Uarabuni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Uarabuni)
Bara Arabu kutoka angani.

Rasi ya Uarabuni (au:Bara Arabu) ni rasi kubwa iliyoko Asia ya Magharibi kati ya Bara la Afrika na Bara la Asia ambapo sehemu yake kubwa imezungukwa na bahari, upande wa magharibi Bahari ya Shamu, upande wa kusini na Bahari ya Hindi na ule wa Mashariki Ghuba ya Uajemi. Sehemu za Kaskazini mwa Bara Arabu zimepakana na nchi za ufalme wa Jordani na jamhuri ya Iraq.

Kwa macho ya gandunia rasi hii ni karibu sawa na bamba la Uarabuni.

Kwa sababu ya ukame, hakuna mito ya kudumu katika bara hili, ijapokuwa kwenye sehemu mbalimbali kunapatikana chemchemi na vijito vya maji ambavyo huzidi wakati wa msimu wa mvua katika majira ya baridi. Sehemu kubwa ni jangwa tu.

Bara Arabu ina milima upande wa Magharibi na Kusini, lakini kila ukiteremkia Mashariki unakutana na ardhi tambarare mpaka kufikia kwenye Ghuba ya Uajemi.

Katika karne ya 20 nchi za Uarabuni zilipata nafasi ya kutajirika kwa sababu ya mafuta mengi ya petroli yaliyo chini ya ardhi yao.

Eneo la Rasi ya Uarabuni

[hariri | hariri chanzo]

Eneo la Bara Arabu kwa jumla ni kilomita mraba 3,191,022, ikiwa Saudia inakalia sehemu nne katika tano ya jumla ya maeneo yake, na sehemu iliyobakia ambayo ni moja katika tano inakaliwa na nchi zilizobakia, zote zikiwepo pembezoni mwa Saudia kwenye bahari ya Ghuba ya Uajemi, bahari ya Kiarabu na bahari ya Shamu.

Nchi za Rasi ya Uarabuni

[hariri | hariri chanzo]

Nchi zilizoko kwenye bara hili ni:

Sita za mwanzo, zikiwemo kwenye Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba, zina mfumo wa kifalme katika utawala wake, na ya mwisho ni Jamhuri ya Yemen.

Nchi hizi zina historia ndefu inayorudi nyuma kabla ya kuja Uislamu, na ustaarabu wa aina mbalimbali ulipatikana katika maeneo ya nchi hizi. Katika ustaarabu mashuhuri wa nchi hizi ni ule ustaarabu wa nchi ya Yemeni, ambao ulikuwa ukijulikana kuwa ni ustaarabu wa Sabaa, zama za Balqis, malkia wa Yemen wakati huo.

Miji Mikuu

[hariri | hariri chanzo]

Kuna miji mingi katika Rasi ya Uarabuni, lakini miji mikuu ya madola mbalimbali ya Rasi ya Uarabuni ni Riyadh, mji mkuu wa Saudia, ijapokuwa kuna miji mashuhuri na mitukufu katika Saudia kama Makka na Madina.

Mji mkuu wa Yemeni ni Sanaa, lakini mingine muhimu ni Aden, Hudeidah, Taez, Mukalla, Shibam na Seyun.

Ama mji mkuu wa Oman ni Maskat, lakini kuna miji mengine mashuhuri yenye tarehe kubwa kama Salala, Sohari, Nizwa na Rustaq.

Mji mkuu wa Falme za Kiarabu ni Abu Dhabi, na mengine mashuhuri ni Dubai, Sharjah, Ajman, Ras-al-Khayma, Ummul-Quwain na Fujairah.

Kuwait, mji mkuu wake ni Kuwait, Qatar mji mkuu wake ni Doha, na Bahrain ni Manama.

Hali ya hewa

[hariri | hariri chanzo]

Rasi ya Uarabuni ina jangwa kubwa la Rub al Khali kusini mwake na An-Nafud kaskazini mwake. Ni sehemu ya ulimwengu ambayo haina mvua nyingi na ukame ndio tabia ya nchi zilizokuwemo katika bara hili. Kwa hivyo, hali ya hewa huwa ni joto sana katika majira ya joto kufikia hadi daraja 55 katika baadhi ya sehemu zake, na kufikia daraja hadi 0 C° katika baadhi ya sehemu nyIngine katika majira ya baridi.

Idadi ya Wakazi

[hariri | hariri chanzo]

Idadi ya wakazi wa nchi hizi saba kwa ujumla inafikia 50,000,000, wakiwemo asilimia 85 wenyeji na asilimia 15 wageni. Wenyeji au wananchi wa nchi hizi aghlabu yake ni Waarabu, lakini pia kuna Waajemi, Mabulushi, Wahindi, Wabangladeshi, Wazungu, Wapakistani, Waafrika na makabila mengineyo.

Nchi zote saba zilizoko kwenye Rasi ya Uarabuni ni za Kiislamu, na aghalabu Waislamu wake ni wa madhehebu ya Sunni, lakini pia kuna madhehebu ya Shia na ya Ibadhi kwenye baadhi ya nchi hizi.

Asilimia 99% ya wananchi wa nchi hizi ni Waislamu, lakini vilevile kati ya wakazi wake, hasa wahamiaji, kuna wafuasi wa dini nyinginezo, kama Wakristo, Mabaniani, Wayahudi na kadhalika.

Kiarabu ndiyo lugha inayotumika kwenye nchi hizi saba, na ndiyo lugha rasmi ya nchi hizi, lakini hivi karibuni Kiingereza kimeanza kutumika sana kwa sababu ya kuwepo dharura ya kutumia lugha hii katika biashara, mawasiliano baina ya wananchi na wageni, na katika uhusiano wa kimataifa baina ya nchi mbalimbali ulimwenguni.

Maliasili

[hariri | hariri chanzo]

Rasi ya Uarabuni ina aina nyingi za madini na nishati. Kuna dhahabu, fedha, chumvi, na kadhalika. Inajulikana hasa kwa akiba zake kubwa za mafuta ya petroli na gesi, jambo lililofanya hizi nchi kutegemea zaidi maliasili hizi kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi zao na maendeleo mengine ya nchi.

Hapo zamani watu wa nchi hizi walitegemea sana uvuvi, ufugaji wa wanyama kama mbuzi, kondoo, ng'ombe, ngamia na farasi. Aidha, walikuwa wakilima na kupanda mitende, matunda, ngano na shayiri, na kwa hivyo, bidhaa zao walizokuwa wakisafirisha nje zilikuwa zaidi ni tende, buni, samaki na papa wakavu, na ngozi za wanyama.

Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Rasi ya Uarabuni kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.