Nenda kwa yaliyomo

Hosea

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha ya nabii Hosea ya karne ya 18, monasteri ya Kizhi, Karelia, Russia.

Hosea (kwa Kiebrania הושע, hoshè'a, yaani "Wokovu") alikuwa nabii katika ufalme wa Israeli (Kaskazini) katika miaka 750 - 725 KK hivi.

Si kwa maneno tu, bali kwa maisha yake pia, alilionyesha taifa kahaba la Israeli jinsi Bwana alivyo Mume daima mwaminifu na mwenye kuongozwa na huruma isiyo na mipaka[1].

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 17 Oktoba[2].

Muda mfupi baada ya Amosi, nabii Hosea alianza kazi yake katika ufalme wa kaskazini, akaweza kuendelea nayo kwa muda mrefu akiwa mwenyeji. Yeye hakufundisha kwa maneno tu, bali hasa kwa maisha yake: mtindo wa kufikirisha kwa matendo ya kushangaza ulitumiwa na manabii wengi, hata na Yesu.

Aliitwa kuoa kahaba ili awaonyeshe Waisraeli katika matatizo ya ndoa yake jinsi Mungu alivyopenda taifa hilo ingawa linapenda kufuata miungu mingine badala ya kuwa aminifu kwake tu. Kwa mfano hai wa Hosea, Mungu alitaka waelewe kwamba kwa kuwapenda na pengine kuwaadhibu analenga tu hatimaye wampende kwa moyo wote.

Sura 1-3 za Kitabu cha Hosea zinasimulia alivyompenda mke wake aliyemzalia watoto wa uzinzi, hata hivyo akaendelea kumpenda na kumtafuta hata baada ya kumfukuza, akamkomboa na kumrudisha ili ambembeleze zaidi na hatimaye amfanye amrudishie upendo kama wakati wa uchumba. Hivyo adhabu yenyewe ilitokana na upendo na kulenga umoja wa dhati.

Hata Mungu, baada ya kuacha Israeli ishindwe na Waashuru, ataendelea na upendo wake kwa wenzao wa kusini, akiwabakiza kama mbegu (ndio “mabaki ya Israeli” yaliyozungumziwa kwanza na Amosi): mpango wa Bwana unapitia hatua mbalimbali lakini haukatiki kamwe.

Mfano huo wa upendo wa Mungu kwa bibiarusi asiye mwaminifu uligusa sana watu ukazidi kuzingatiwa mpaka katika Agano Jipya na kuchangia uimara wa ndoa iliyofikiriwa upya kama upendo mwaminifu, si kama uhusiano wa kisheria au wa kimwili tu ambao udumu mpaka utakapoendelea kuleta faida. Zaidi ya hayo, uliwaelekeza Waisraeli kupokea fundisho la Yesu kwamba dini ni suala la upendo, si ibada wala sheria tu.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hosea kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.