Heri Nane
Heri Nane ni kauli maarufu za Yesu Kristo zilivyoandikwa katika Injili ya Mathayo (5:3-12).
Zikiwa zimepangwa mwanzoni kabisa mwa Hotuba ya mlimani na mafundisho yote ya Yesu, ni kati ya maneno yake muhimu zaidi na ambayo yameathiri zaidi maisha ya wafuasi wake na hata ya watu wengine, kama Mahatma Gandhi.
Maneno yenyewe
[hariri | hariri chanzo]Kwa Kigiriki, lugha asili ya Injili, zinasema hivi:
3Μακάριοι οἱ πτωχοὶ τῷ πνεύματι· ὅτι αὐτῶν ἐστιν ἡ βασιλεία τῶν οὐρανῶν.
4Μακάριοι οἱ πενθοῦντες· ὅτι αὐτοὶ παρακληθήσονται.
5Μακάριοι οἱ πραεῖς· ὅτι αὐτοὶ κληρονομήσουσιν τὴν γῆν.
6Μακάριοι οἱ πεινῶντες καὶ διψῶντες τὴν δικαιοσύνην· ὅτι αὐτοὶ χορτασθήσονται.
7Μακάριοι οἱ ἐλεήμονες· ὅτι αὐτοὶ ἐλεηθήσονται.
8Μακάριοι οἱ καθαροὶ τῇ καρδίᾳ· ὅτι αὐτοὶ τὸν Θεὸν ὄψονται.
9Μακάριοι οἱ εἰρηνοποιοί· ὅτι αὐτοὶ υἱοὶ θεοῦ κληθήσονται.
10Μακάριοι οἱ δεδιωγμένοι ἕνεκεν δικαιοσύνης· ὅτι αὐτῶν ἐστιν ἡ βασιλεία τῶν οὐρανῶν.
Tafsiri mojawapo ya Kiswahili ni hii:
3 "Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
4 Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa.
5 Heri walio wapole, maana watairithi nchi.
6 Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa.
7 Heri walio na huruma, maana watahurumiwa.
8 Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu.
9 Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu.
10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
11 Heri yenu ninyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu.
12 Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu.
Ufafanuzi wa Mababu wa Kanisa[1]
[hariri | hariri chanzo]Hotuba ya mlimani ni muhtasari wa mafundisho aliyoyatoa Mwokozi ili kutimiliza sheria ya Musa na kusahihisha ufafanuzi wake usiofaa. Heri nane alizotangaza mwanzoni mwa hotuba hiyo zinaonyesha ukamilifu anaowaitia wote na zinajumlisha vizuri ajabu kipeo cha maisha ya Kikristo katika ukuu wake wote.
Neno la kwanza la Yesu ni kuahidi heri na kuelekeza njia za kuipata. Alianza na heri kwa sababu kila mtu kwa umbile lake anaitamani: ndiyo lengo ambalo wote, watake wasitake, wanalitafuta katika yote. Lakini mara nyingi wanatafuta heri isipokuwepo, watakapokuta tu mahangaiko na unyonge. Yeye anatuambia heri halisi ya kudumu na lengo la maisha yetu viko wapi, tena anatupatia njia za kuvipata. Lengo linaloelekezwa kwa majina mbalimbali ni ile heri ya milele ambayo waadilifu wanaanza kuionja hapa duniani: ni ufalme wa Mungu, nchi ya ahadi, faraja kamili, utimilifu wa hamu zote zilizo halali na takatifu, rehema kuu, kumuona Baba yetu. Njia zinakwenda kinyume cha maelekezo ya ulimwengu, kwa kuwa lengo ni tofauti mno.
Mpangilio wa heri nane unaanzia chini kwenda juu, kinyume na sala ya Baba Yetu ambayo kisha kuzingatia utukufu wa Mungu inateremkia mahitaji yetu.
- Heri tatu za kwanza ni zile zinazopatikana katika kukwepa dhambi na kukombolewa: katika ufukara uliopokewa kwa upendo wa Mungu, katika upole na katika machozi ya majuto.
- Heri mbili zinazofuata ni zile za maisha ya utendaji ya Kikristo: zinahusu kiu ya haki na utekelezaji wa huruma kwa jirani.
- Halafu zinakuja zile za kuzama katika mafumbo ya Mungu: usafi wa moyo unaotuandaa kumuona na amani inayotokana na hekima ya kweli. Heri ya mwisho na bora kuliko zote ni ile inayoziunganisha zilizotangulia hata wakati wa kudhulumiwa kwa ajili ya haki.
Heri za ukombozi kutoka dhambi
[hariri | hariri chanzo]Hizo zinahusu hatua ya utakaso, ambayo ni maalumu kwa wanaoanza.
Ulimwengu unasema heri inapatikana katika utajiri na heshima. Kumbe Bwana amesema wazi, kwa hakika tulivu ya ukweli, “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Math 5:3). Kila heri ina viwango mbalimbali: heri walio fukara bila kunung’unika, kwa uvumilivu, bila kijicho, hata wakikosa chakula, na wanaofanya kazi wakimtegemea Mungu tu. Heri waliobahatika zaidi, lakini hawana roho ya utajiri, fahari, kiburi, wala hawashikamani na mali. Heri zaidi walioacha vyote ili kumfuata Yesu, wakijifanya fukara kwa hiari na kuishi kweli wito huo; hao watapata mara mia hapa duniani halafu uzima wa milele. Fukara hao, kwa kuvuviwa kipaji cha uchaji, wanafuata njia nyembamba ambayo baadaye inakuwa barabara kuu ya mbinguni, roho inapozidi kutanuka, wakati njia pana za ulimwengu zinaelekea maangamizi: “Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa” (Lk 6:25). Kumbe, ufukara wenye heri unatufungulia ufalme wa Mungu, ulio bora kuliko mali yoyote, yanavyoonyesha maisha ya Fransisko wa Asizi. Heri wanyenyekevu wa moyo, wasiojitwalia mema ya kimwili wala ya Kiroho, wala heshima wala upendo, bali wanatafuta ufalme wa Mungu tu.
Tamaa ya utajiri inatenganisha watu na kusababisha ugomvi, mashtaka, kesi, dhuluma na hata vita kati ya mataifa. Kumbe Yesu amesema, “Heri wenye upole, maana hao watairithi nchi” (Math 5:5). Heri wasiokasirikia ndugu zao, wasiotaka kulipa kisasi wala kutawala wengine, wasiohukumu bila msingi, wasiomuona jirani kama adui wa kushindana naye, bali kama ndugu wa kusaidiwa. Kipaji cha ibada ndicho kinachotutia upole huo kwa pendo la kitoto kabisa kwa Mungu, Baba yetu sote. Wapole hawashikamani mno na mtazamo wao wala hawaoni haja ya kuapa kwa chochote kile. Ili tuwe hivyo hata kwa wanaotutendea ukali, tunahitaji kuungana na Yesu aliyesema, “Mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Math 11:29). Yeye hakuvunja “mwanzi uliopondeka” wala kuzima “utambi utokao moshi” (Math 12:20) akafananishwa na “mwanakondoo apelekwaye machinjoni” asifunue “kinywa chake” (Isa 53:7; Mdo 8:32). Upole huo si ule unaostahili lawama ambao kwa woga haumchukizi yeyote, bali ni adili linalotegemea upendo mkubwa kwa Mungu na kwa jirani: unazidisha thamani ya huduma unayotoa, unaweza kusema lolote na kufanya mtu apokee mashauri na hata shutuma kwa kutambua vinatokana na upendo. Heri walio wapole, maana watarithi nchi halisi ya ahadi, na tangu sasa wanajipatia kitakatifu mioyo ya wale wanaojiaminisha kwao.
Ulimwengu unasema furaha inapatikana katika anasa. Kumbe Yesu amesema, “Heri wenye huzuni, maana hao watafarijika” (Math 5:4). Ndivyo tajiri alivyojibiwa: “Wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa” (Lk 16:25). Heri wale ambao, kama Lazaro, wanateseka kwa subira, bila kufarijiwa na watu; ila Mungu anaona machozi yao. Wenye heri zaidi wanaolia juu ya dhambi zao, ambao kwa kipaji cha elimu wanang’amua kwamba dhambi ndiyo jambo baya kuliko yote, na wanajipatia msamaha kwa kulia machozi. Zaidi tena wana heri wanaolia kwa upendo, wakizingatia huruma na hisani zisizo na mipaka za Mchungaji mwema aliyejitoa sadaka kwa kondoo zake. Hao wanapokea farajia isiyo na kifani kuanzia hapa duniani.
Heri za maisha ya utendaji ya Kikristo
[hariri | hariri chanzo]Mwadilifu ambaye, kisha kuopolewa maovuni, anajitahidi kutenda mema kwa moyo wote, ameandaliwa furaha nyingine takatifu.
Anayetawaliwa na kiburi anamuita mwenye heri yule anayeishi na kutenda anavyotaka, asiyekaa chini ya wengine bali anawashinda. Kumbe Yesu amesema, “Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa” (Math 5:6). Maana pana ya neno “haki” ni kumpatia Mungu yale anayostahili; hapo kwa upendo wake hata watu wanapatiwa wanayostahili. Kama malipo Mungu anajitoa kwetu. Ndio utaratibu kamili katika utiifu ambao unaongozwa na upendo unaopanua moyo. Wenye heri wanaotamani haki hiyo hadi kuwa na njaa na kiu nayo. Kwa namna fulani watashibishwa kuanzia hapa duniani, kwa kugeuka watakatifu. “Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe… mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake” (Yoh 7:37-38). Lakini ili tudumishe kiu hiyo hata katikati ya ukavu wa hisi, upinzani, vizuio, kukabili ukweli, ni lazima tupokee kwa mikono miwili kipaji cha nguvu, kinachotutia moyo katika matatizo tusishindwe wala tusikate tamaa. “Bwana anataka tuitamani haki hiyo hivi kwamba tusishibe kamwe hapa duniani, kama vile mroho asivyoshiba kamwe… Tutashiba tutakapomuona Mungu milele… na tangu sasa katika mema ya Kiroho… Watu wakiwa katika dhambi, hawasikii njaa ya Kiroho, ila wanapoacha dhambi wanaisikia” (Thoma wa Akwino).
Lakini njaa na kiu ya haki haitakiwi kuendana na ari chungu kuhusu wakosefu: “Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” (Math 5:7). Katika maisha yetu, kama vile kwa Mungu, haki inapaswa kuungana daima na huruma. Hatuwezi kuwa wakamilifu tusipomsaidia mwenye uchungu au ugonjwa kama alivyofanya Msamaria mwema. Bwana atawalipa wanaojitolea bilauri ya maji kwa upendo wake, wanaokaribisha mezani pao fukara, walemavu na vipofu. Mkristo anapaswa kufurahia zaidi “kutoa kuliko kupokea” (Mdo 20:35), tena kusamehe (kwa Kilatini “perdonare”, yaani “kutoa zaidi”) waliomchukiza, kusahau dharau na kupatana na nduguye kabla hajatolea altareni sadaka yake. Kipaji cha shauri kinatuelekeza kwenye huruma, na kututambulisha mateso ya wenzetu pamoja na dawa yake, k.mf. neno la kuwainua na kuwafariji.
Ikiwa mara nyingi utendaji wetu utafuata maadili hayo mawili ya haki na huruma, pamoja na vipaji vinavyohusiana nayo, tutajaa furaha takatifu tokea hapa duniani na kuwa tayari kuingizwa katika mafumbo ya Mungu.
Heri za kuzama ndani ya Mungu na kuungana naye
[hariri | hariri chanzo]Baadhi ya wanafalsafa waliona heri inapatikana katika kujua ukweli, lakini hawakujali usafi wa moyo, ikawa maisha na mafundisho yao yalipingana katika mambo kadhaa. Kumbe Yesu amesema, “Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu” (Math 5:8). Hakusema wana heri walio na akili sana pamoja na muda na njia za kuistawisha, bali wenye moyo safi, hata kama kimaumbile akili yao ni ndogo kuliko ya wengine. Hao watamuona Mungu: ni kama maji safi ya ziwa ambamo uangavu wa anga unarudishwa, au kama kioo cha Kiroho ambamo sura ya Mungu inaonekana. Lakini usafi wa moyo unadai kujifisha kwa bidii: “Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe… Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe” (Math 5:29-30). Tunapaswa kuangalia hasa tuwe na nia njema: si kutoa sadaka mbele ya watu ili kuonekana nao, wala kusali ili kusifiwa nao, bali kutafuta tu tumpendeze Baba “aonaye sirini” (Math 6:4,6,18). Hapo tu yatatimia maneno ya Mwalimu: “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru” (Math 6:22). Tokea hapa duniani Mkristo atamuona Mungu kwa namna fulani katika majirani, hata katika watu wanaompinga; atamuona katika Maandiko Matakatifu, katika maisha ya Kanisa, katika nafasi mbalimbali za maisha yake mwenyewe, hata katika majaribu, ambapo atajifunza maongozi ya Mungu. Ndipo sala ya kumiminiwa inapopatikana kwa msaada wa kipaji cha akili, tunapojiandaa kumuona Mungu na uzuri wake usiopimika; hapo hamu zetu zote zitatimia, nasi tutakuwa kama tumeleweshwa na mto wa vitamu vya Kiroho.
Tangu hapa duniani huko kuzama ndani ya Mungu kunazaa matunda; kunaleta amani angavu, inavyotangaza heri ya saba: “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Math 5:9). Heri hiyo inahusiana na kipaji cha hekima kinachotufanya tuonje mafumbo ya milele, na kuona kwa namna fulani mambo yote ndani ya Mungu. Polepole miangaza ya Roho Mtakatifu, ambayo kipaji hicho kinatusaidia kuipokea kwa mikono miwili, inatuonyesha utaratibu mzuri ajabu wa maongozi ya Mungu, pengine palepale - na hasa pale - tulipopatwa kwanza na mshtuko mkubwa katika matukio machungu yasiyotarajiwa ambayo Mungu aliyaruhusu kwa manufaa makubwa zaidi. Hatuwezi kung’amua hivyo jinsi anavyoongoza maisha yetu bila kufaidi amani kubwa. Ili tusifadhaishwe na matukio hayo, bali tuyapokee yote mikononi mwa Mungu kama njia ya kumuendea, ni lazima kujiachilia kwa Roho Mtakatifu, anayetaka kutujalia hatua kwa hatua kutazama mambo ya Kimungu, ambako ni sharti la kuungana naye. Ndiyo sababu ametujalia kipaji cha hekima. Miangaza yake inatupatia amani angavu, si kwa ajili yetu tu, bali kwa jirani pia; inatufanya wenye amani; inatusaidia kuwapa amani watu wasiotulia, kuwapenda maadui, kusema maneno ya upatanisho yanayomaliza ugomvi. Hiyo amani ambayo ulimwengu hauwezi kuitoa, ndiyo ishara ya watoto halisi wa Mungu ambao hawaachi kumfikiria Baba wa mbinguni.
Hatimaye, katika heri ya nane, Bwana ametuonyesha kwamba yale yote aliyoyasema yanathibitishwa hasa na majaribu yaliyovumiliwa kwa upendo: “Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Math 5:10). Ndiyo hasa majaribu ya mwisho yaliyo masharti ya utakatifu. Halijasikika neno la kushangaza kama hilo ambalo halituahidii heri milele tu, bali pia wakati wa uchungu na dhuluma. Ni heri isiyo ya kimaumbile hata kidogo, inaeleweka tu na wale walioangazwa na Mungu. Ndani yake kuna ngazi nyingi, kuanzia ile ya Mkristo anayeanza kuteseka kwa kuwa ametenda mema, ametii, ametoa mfano mzuri, hadi ile ya mfiadini. Heri hiyo inamhusu mwongofu anayepingwa tu katika mazingira yake; pia mtume ambaye kazi yake inazuiwa na walewale anaotaka waokoke, wasiokubali kumsamehe kwamba anawaeleza wazi kweli za Injili. Pengine makabila mazima yanapaswa kustahimili dhuluma za namna hiyo. Heri hiyo ni kamili kuliko zote kwa sababu ni ya wale wanaofanana zaidi na Yesu msulubiwa. Kudumu wanyenyekevu, wapole na wenye huruma wakati wa dhuluma, hata kwa watesi wenyewe, na si tu kuendelea kuwa na amani, bali kuwashirikisha wengine pia, ndio ukamilifu wa Kikristo. Si watakatifu wote walifia dini, lakini kwa viwango tofauti wote walidhulumiwa kwa ajili ya haki na kung’amua walau kidogo ule ushahidi wa moyoni uliomfanya Maria Mama wa huzuni. Yesu alisisitiza tuzo waliloahidiwa watu hao, “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni” (Math 5:11-12). Kutokana na maneno hayo Inyasi wa Antiokia na wengineo walitamani kufia dini. Ndiyo sababu wakawa “chumvi ya dunia” na “nuru ya ulimwengu” (Math 5:13-14), na nyumba yao, iliyojengwa juu ya mwamba, ilistahimili dhoruba zote isianguke.
Heri hizo ni matendo bora ya maadili yaliyokamilishwa na vipaji, hivyo zinapita juhudi zetu na kutegemea mafumbo. Kwa maneno mengine, ukamilifu wa Kikristo ni mwanzo wa uzima wa milele, tutakapokuwa wakamilifu kama Baba, tukimuona na kumpenda kama mwenyewe anavyojiona na kujipenda. Teresa wa Yesu aliandika, “Vitabu kadhaa vinasema tusijali mabaya yanayosemwa juu yetu, bali tuyafurahie kuliko maneno ya sifa, tusijali sana heshima tunayopewa, tusishikamane na ukoo… na sijui mambo mangapi ya namna hiyo… Nionavyo mimi, hayo ni zawadi za Mungu tu, ni mema yanayopita maumbile”, yaani yanapita uwezo wa juhudi zetu katika kutekeleza maadili; ni matunda yanayozaliwa na usikivu mkubwa kwa Roho Mtakatifu. “Tukipenda heshima na tunu za kidunia, hata tukisali, au afadhali niseme tukitafakari miaka na miaka, hatutaendelea kweli kamwe. Kumbe sala kamili inatukomboa kutoka kasoro hizo”. Maana yake pasipo sala ya kumiminiwa hatuwezi kuufikia ukamilifu.
Ndivyo ilivyoandikwa katika Kumfuasa Yesu Kristo, “Utakapofaulu kujidharau kabisa, uwe na hakika kwamba umepata kuonja amani yote inayowezekana hapa duniani” (III,25:3). Ndiyo sababu mwanafunzi anaomba kumiminiwa sala, “Mungu wangu, nahitaji sana neema kubwa zaidi, ikinipasa kufikia hali njema nisiweze kuzuiwa tena na kiumbe chochote… Mtu aliyetamani kuruka afike kwako, alisema, Nani atanipa mabawa kama ndege nipate kuruka na kufika mustarehe? Mtu asiyevunja vifungo vinavyomfunga pamoja na viumbe, hatapata nafasi ya kumfikiri Mungu na mambo yake. Ndiyo maana hatuoni watu wengi wa kuzama ndani ya Mungu, kwa kuwa wenye kujitenga kabisa na mambo mapotevu ya dunia au hata na viumbe vyote huwa wachache. Kufanya hivi hutaka neema kubwa sana, yenye kuinua roho na kuivuta ipae juu ya hali yake. Lakini kama mtu hapandi vile rohoni mwake kwa kujitenga na viumbe vyote aambatane na Mungu tu, yote ayajuayo na yote awezayo hayana maana” (III,31:1-2).
Ustawi huo kamili wa muundo wa Kiroho, yaani wa neema ya maadili na vipaji, unaonyeshwa katika heri nane si kinadharia tu, bali katika utekelezaji wake.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Hasa Augustino wa Hippo
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Heri Nane kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |