Msimbo pau
Msimbo pau ni ruwaza ya kijiometri, kwa kawaida ni mistari iliyo wima, ambayo hutumiwa kukagua na kufuatilia mali au bidhaa. Ni njia ya kutaja namba inayoruhusu kusomewa kwa namba hizi kwa mashine.
Awali msimbo pau ulitumia ufuatano wa mistari au "pau" sambamba na nafasi iliyopo baina ya mistari sambamba. Mfumo huu sahili unaitwa kimstari (linear) au wa wanda moja (one-dimensional / 1D).
Baadaye msimbo wa wanda mbili (2D) ulianzishwa, kwa kutumia mistatili, nukta, pembe sita na ruwaza nyingine za kijiometri katika pande mbili, kawaida huitwa misimbo pau ingawa haitumii pau.
Awali Misimbo pau ilikaguliwa kwa vitambazo mwanga maalum vilivyoitwa "barcode readers". Baadaye programu tumizi, maarufu kama protu(software aplications) zilipatikana katika vifaa ambavyo viliweza kusoma picha, kama vile simujanja (smartphones) na kamera.
Ingawa mwanzo msimbo pau ulitumika kufuatilia magari ya reli, ulipata umaarufu zaidi wakati ulipokuja kutumika kwenye bidhaa zinazouzwa katika maduka makubwa penye kifaa cha kusoma msimibo pau.
Zipo aina mbili za misimbo pau, msimbo wa bidhaa wa jumla (Universal Product Code - UPC) na International Standard Book Number (ISBN), ambazo ni lazima kuombwa kupitia mashirika rasmi ya uhakikishaji wa bidhaa kabla ya kuuzwa.
Misimbo pau inaweza kutumika kwa kufuatilia hesabu ya bidhaa za rejareja, au kutumika binafsi kuweka misimbo na kufuatilia makusanyo au bidhaa.
UPC
[hariri | hariri chanzo]UPC (kitaalam inahusu UPC-A) ina tarakimu 12 za namba, ambayo kipekee hutolewa kwa kila bidhaa ya biashara. UPC ni msimbo pau utumikao hasa kwa ajili ya ukaguzi wa vitu vya biashara wakati wa kuuza.
Kila msimbo pau wa UPC-A una ukanda unaoweza kutambazwa wa pau nyeusi na nafasi nyeupe juu ya mtindo wa tarakimu wa namba 12. Hakuna herufi, alama au maudhui mengine ya aina yoyote yanayoweza kuonekana kwenye msimbo pau wa UPC-A.
ISBN
[hariri | hariri chanzo]International Standard Book Number (ISBN) ni namba ya kipekee ya utambulisho wa vitabu viuzwavyo kibiashara.
ISBN inapangwa kwa kila toleo na tofautisho (isipokuwa marekebisho) la kitabu. Kwa mfano, Kitabu cha kielektroniki, paperback na toleo gumu (hardcover) la kitabu kilekile kila moja itakuwa na ISBN tofauti. ISBN ina urefu wa tarakimu 13 kama ingewekwa siku au baada ya tarehe 1 Januari 2007, na urefu wa tarakimu 10 kama ingewekwa kabla ya mwaka 2007.
Namna ya kuwekaji wa ISBN inategemea taifa lenyewe na hutofautiana kutoka nchi hadi nchi, mara nyingi inategemea na ukubwa wa sekta ya uchapishaji ndani ya nchi.